Friday, 12 February 2016

Tanzania yakiuka Mkataba wa Kimataifa wa haki ya mtoto Gerezani.

Na Mkombe Zanda,
Mbeya.

Licha ya Tanzania kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, CRC, unaozuia kuwachanganya watoto na watu wazima gerezani lakini bado kuna watoto wengi wanaokaa magerezani kote nchini kinyume na mkataba huo.

Mbali na kuridhia Mkataba huo wa Kimataifa, Tanzania pia imeunda Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ili kulinda haki za mtoto lakini bado juhudi hizo hazijafanikiwa kuondoa uwezekano wa watoto kuishi magerezani kinyume na matakwa ya kisheria.

Kushindwa kwa Tanzania kutekeleza ipasavyo mkataba huo wa Kimataifa na sheria hiyo iliyoundwa nchini, kumebainishwa jijini Mbeya na Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Haki za Mtoto na Marekebisho ya Tabia kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Rabikira Mushi katika mahojiano na Star Tv wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Marekebisho ya Tabia na Mpango wa Utoaji Msaada wa Sheria kwa Watoto Wanaokinzana na Sheria.

Chanzo cha hali hii kinaonekana ni ukosefu wa mahabusu za watoto kote nchini.

Kimsingi kesi zinazowahusu watoto hapa nchini zinashughulikiwa na Hakimu Mkazi wa eneo husika, hivyo baadhi ya wadau wa haki za watoto wamependeza kuwa kesi hizo sasa zishughulikiwe na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo ili kupunguza urasimu na idadi ya watoto wanaokaa gerezani.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Child Protection Budget Identification Survey mwaka 2012 unaonesha kuwa Halmashauri za Tanzania zinatenga asilimia 0.002 ya bajeti zao za kila mwaka kama fedha za kushughulikia haki za watoto kiasi ambacho hakitoshi kukabiliana na changamoto zilizopo.

No comments:

Post a Comment